Iraq inatakiwa ianzishe opereshini za kijeshi kuukomboa mji muhimu wa kaskazini-Mosul unaodhibitiwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh,huku Marekani na Uturuki zikikubaliana kuwapatia mafunzo waasi wa Syria
Kikosi cha wanajeshi wa Iraq na kikurdi wapatao 25 elfu wanatayarishwa ili kuweza kuukomboa mji wa Mosul unaodhibitiwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh. Uongozi wa kijeshi wa Marekani uliotangaza habari hizo unakadiria mji huo wa Mosul unadhibitiwa na wapiganaji kati ya 1,000 na elfu mbili wa kundi la kigaidi la Daesh. Hakuna bado uamuzi uliopitishwa kama idadi ndogo ya washauri wa kijeshi wa Marekani watahitajika katika eneo la karibu na Mosul ili kusaidia opereshini za ndege za kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh.
Mosul, mji wenye wakaazi zaidi ya milioni moja ulitekwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh mwezi juni mwaka jana na ni mji mkubwa kabisa kutangazwa Dola ya Kiislamu - au Khalifa, unaoanzia kaskazini ya Iraq na kupakana pia na eneo la mashariki la Syria.
Kikosi kilichotengwa kwaajili ya opereshini hizo kitaundwa na vikundi vitano vya jeshi la Iraq-uongozi wa kijeshi wa Marekani umesema.Vikosi vitatu vitatumika kama akiba na vikosi vyengine vitatu vya wapiganaji wa kikurd-Peshmerga watakuwa na jukumu la kuzuwia njia za kuingia kaskazini ya Mosul na kuwazingira wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh waliopiga kambi magharibi ya mji huo.
Kikosi chengine pia kinaundwa wakihusishwa wanamgambo wa kikabila pamoja na kundi la wanajeshi watakaokuwa na jukumu la kupambana na ugaidi.
Tarehe halisi ya kuanza opereshini hizo itategemea na jinsi maandalizi yanavyoendelea upande wa Iraq.
Ni nadra kwa jeshi la Marekani kutoa maelezo kuhusu ratiba ya opereshini za kijeshi,lakini wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imejieleza kwa kusema ripoti hii inabainisha jeshi la Iraq ni la kuaminika.
Juhudi za kuwavunja nguvu kundi la kigaidi la Daesh zimepamba moto
Marekani na Uturuki zimetiliana saini makubaliano ya kuwapatia mafunzo na vifaa vya kijeshi waasi wa Syria wanaofuata msimamo wa wastani nchini Uturuki ili waiangushe Serikali ya Syria. Habari hizo zimetangazwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglo mbele ya waandishi habari mjini Ankara. Makubaliano hayo yamekamilisha miezi kadhaa ya majadiliano magumu kati ya washirika hao wawili wa jumuia ya kujihami ya NATO kuhusu namna ya kupatiwa mafunzo waasi wa Syria na adui yupi anastahiki kulengwa.
Marekani ambayo jeshi lake la wanaanga linashiriki katika opereshini dhidi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh inapendelea kuwapatia mafunzo waasi ili wajiunge na mapambano dhidi ya serikali ya Syria. Washington inataraji mafunzo hayo yataanza kutolewa mwezi ujao wa Marchi ili kuwawezesha washirki katika mapambano dhidi ya serikali ya Syria hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu.
Hapo awali Marekani na washirika wake walilipa nguvu na kulisaidia kundi la kigaidi la Daesh ili liiangushe serikali ya Syria, lakini baada ya kundi hilo kwenda kinyume na maslahi ya Marekani na washirika wake kundi hilo limetangazwa kuwa ni kundi lenye misimamo mikali na kuwa ni kundi la kigaidi, hivyo kwa sasa Marekani na Uturuki wanatengeneza kundi jingine ambalo halitakuwa na misimamo mikali ili litimize malengo yao ya kuiangusha serikali ya Syria ambayo ni moja kati ya maadui wakubwa wa Israel na mshirika wa karibu wa Jamhuri ya kiislamu ya Iran.
Njama za kijeshi za Marekani na washirika wake zimeshindwa katika kuingusha serikali ya Syria baada ya kukutana na jeshi la Iran na Hizbullah ambazo zinapambana kuitetea serikali halali ya Syria, hapo awali makundi yanayopata udhamini kutoka kwa Marekani na washirika wake yalitangaza kuiangusha serikali ya Syria katika kipindi kisichozidi miezi sita, lakini imefika miaka minne mpaka sasa wameshindwa kufikia lengo lao, hii inatokana na uwezo wa jeshi la Syria likishirikiana na majeshi ya Iran na Hizbullah.